PACSO: ‘TUNATEKELEZA KWA VITENDO MAONO YA DK. MWINYI, DK. SAMIA’

MRATIBU wa miradi kutoka Mwenvuli wa asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, alisema wanatekeleza kwa vitendo, maono ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha elimu ya uraia na demomkrasia inawafikia wananchi.

Mratibu huyo aliyasema hayo, wakati akizungumza na watendaji wa serikali na wanaasasi za kiraia, katika kongamano la pamoja, la kujenga ushirikiano, baina pande mbili hizo, kupitia mradi wa ‘uraia wetu’ lililofanyika Wawi Chake chake.

Alisema, mradi huo ni tokeo moja wapo la maono ya viongozi hao, ambapo wameamua kuwakusanya watendaji wa serikali na wale wa asasi za kiraia, ili kuibua changamoto zinazokwamisha ushirikiano wao.

Alieleza kuwa, washiriki wa kongamanio hilo, watapata nafasi ya kuelezea changamoto zao kikanuni, sera na kisheria ili kuona zinatatuliwaje kwa umoja wao.

‘’Sote ni mashahidi kuwa, wakati viongozi wetu wanaingia madarakani, walihimiza mno suala la kuzifahamu sheria, kuona changamoto zake na hata kuzifanyia marekebisho, ili kusiwe na mkwamo katika utekelezaji wa shughuli husika,’’alieleza.

Aidha Mratibu huyo wa miradi kutoka ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, alieleza kuwa washiriki watachambua sera, kanuni na sheria ambazo wakati wanapotekeleza majukumu yao, zinawakwaza.

 

 

Katika hatua nyingine alifafanua kuwa, PACSO imeandaa jukwaa la kuwakutanisha pamoja watendaji wa serikali na wanaasasi za kiraia, ili kujadili kwa pamoja changamoto za watu wenye ulemavu, vijana na wanawake.

Alieleza kuwa, maoni ambayo yatapatikana katika kongamano hilo, watayaandika vyema na kuyasilisha kwa Jumuiya ya wanawake wanawake wenye ulemavu Zanzibar, ambao nao watakeleza mradi kama huo, ngazi ya kitaifa.

‘’Kwenye mradi huu PASCO, inatekeleza ngazi ya kanda (zone), ingawa wenzetu wa JUWAUZA wanatekeleza ngazi ya kitaifa na kisha maoni hayo, watayafikisha kwa viongozi wa kitaifa,’’alieleza.

Akifungua kongamanio hilo, Msaidizi Naibu Mrajisi wa Asasi za Kiraia Pemba, Saada Abubakar Khamis, alisema mradi huo, unaweza kuleta tija, kwa vile unaangalia kwa upana wake, suala la demokrasia.

Alieleza kuwa, moja ya chanagamoto iliyopo ni kutoonekana kwa uhusiano mzuri, baina ya asasi za kiraia na serikali kuu, jambo ambalo wakati mwengine huchelewa kutekelezwa kwa miradi.

‘’Jambo hili lililofanywa na wenzetu ‘PACSO’ naamini litazidisha ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali na asasi za kiraia, hasa kwa vile pia litaangalia sheria na kanuni zinazokwamisha utendaji wa asasi,’’alifafanua.

Alifafanua kuwa, demokrasia ni dhana pana na wakati mwengine wapo wanaoona inahusu ngazi za juu pekee, bila ya kuona kuwa dhana hiyo, hutakiwa kuonekana hata kwenye asasi za kiraia.

Wakichangia kwenye kongamano hilo, washiriki hao walisema ushirikishwaji ni jambo jema, katika kufikia uamuzi wowote, katika nchi ama asasi za kiraia.

Afisa wa watu wenye ulemavu wilaya ya Chake chake Mwadini Ali Juma, alisema bado watu wenye ulemavu, hawajatendewa haki sana katika ajira, miundombinu na majengo ya umma.

Mwakilishi kutoka TAMWA, Asha Mussa Omar, alisema kikwazo kilichopo ni kwa jamii, kutotaka kubadili mitazamo, juu ya dhana ya mwanamke na uongozi.

‘’Wapo baadhi ya watu wanawavunja moyo wanawake, kwa kuwaambia kuwa wakiwa viongozi, watakuwa wamevunja maadili, watapewa takala, dhana hizi zinahitaji elimu kwa bidii,’’alieleza.

Akiwasilisha mada ya umuhimuwa ushirikiano baina ya asasi za kiraia na serikali, mkufunzi Juma Bakar Alawi, alisema hakuna haja ya pande mbili hizo, kunyimana taarifa.

Alieleza kuwa, asasia zote za kiraia Zanzibar, zinatekeleza miradi ambayo ni maono ya serikali kuu, hivyo ni vyema pande moja wapo inapohitaji taarifa, iwe rahisi kupeana.

Kongamano hilo la siku moja, kupitia mradi wa ‘uraia wangu’ limeandaliwa na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society kupitia Umoja wa nchi za Ulaya.