PACSO YAWAONESHA NJIA YA MALEZI WAZAZI, WALEZI PEMBA

JAMII kisiwani Pemba, imetakiwa kufahamu changamoto na viashiria vya udhalilishaji kwa watoto, ili kuwalinda na vitendo hivyo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Pemba ‘PACSO’ Mohamed Ali Khamis, mara baada ya kuutambulisha mradi wa kujadili changamoto zinazowakabili watoto, katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Pemba.

Alisema, jamii inapaswa kuwa karibu mno na watoto wao, ili kujua haraka viashiria vya kudhalilishwa, na sio kusubiri hadi janga liwakumbe.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, hilo litakuwa rahisi ikiwa wazazi na walezi watatenga muda wa kuwa karibu na watoto wao.

‘’Kama tunajiona tuko na harakati nyingi za maisha na kusahau kukaa na watoto wetu, wanaweza kukumbwa na janga kama la udhalilishaji na tukachelewa kufahamu,’’alieleza.

Akielezea lengo la mradi huo Mwenyekiti huyo wa PACSO, alisema ni kuwazindua wazazi, kufahamu viashiria na changamoto na namna ya kuwasaidia watoto wasifanyiwe matendo hayo.

Akifungua mafunzo hayo, Mratibu katika ofisi ya usajili wa asasi za kiraia Pemba, Ashrak Hamad Ali, alisema baadhi ya wazazi wanakosa muda wa kukaa na watoto wao, ili kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Aidha aliwataka wazazi kujenga utamaduni wa kukaa na watoto wao ili kuwapa fursa ya kuwasikiliza sambamba na kufuatilia nyenendo zao za kila siku.

Katika hatua nyingine, Mratibu huyo, aliwataka waandishi wa habari kushirikiana na viongozi wa dini, kutoa elimu kwa wanandoa, ili kupunguza talaka za kiholela.

‘’Wakati mwengine wapo watoto wetu wanakumbana na changamoto za kimaisha na kisha kudhalilishwa ama kutelekezwa, moja ya sababu ikiwa ni wazazi kutengana,’’alifafanua.

Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo kuhusu changamoto zinazowakabili watoto, Mratibu kutoka Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA– Pemba Fat- hyia Mussa Said, alisema watoto wana haki ya kushiriki na kushirikishwa kwenye ngazi za kijamii.

Akizitaja baadhi ya haki hizo kupitia mkataba wa kimatifa wa mwaka 1988 ni pamoja na ya kuishi, kuendelezwa kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya mtoto Tanzania, kulindwa na vitendo viovu pamoja na haki ya kushirikishwa.

Nao washiriki wa mkutano huo, Aisha Abdallah Juma na mwenzake Abdurr-azak Imam Juma, walisema ni hatari kwa wazazi kupuuzi taarifa wanazopewa na watoto wao.

Sheha wa shehia ya Pembeni wilaya ya Wete Saumu Ali Hamad na mjumbe wa sheha shehia ya Wambaa Amini Haji Makame, walisema kukosekana kwa uthubutu wa wazazi, kuwakemea watoto kuiga mitindo ya kigeni ni moja ya chanzo cha kutokea kwa changamoto hizo.

Awali, Mratibu wa miradi kutoka PACSO Mohamed Najim Omar, alisema kama jamii haikuungana kama ilivyokuwa zamani kwenye malezi, watoto wataendelea kukumbwa na changamoto.

Aidha aliwataka washiriki wa mkutano huo, kuisambaaza elimu walioipata, ili kuona wazazi na walezi wanakuwa na mamko wa malezi kwa watoto wao.

Mradi huo wa miezi sita unatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Irish Aid, unaendeshwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Pemba ‘PACSO’.